HATIMAYE watoto wawili wa Sophia Rashidi (22) ambao ni Omari Rashid (4)
na Maulid wa miezi kumi, waliolazwa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya
Fahamu (Moi) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wamefanyiwa
upasuaji.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita
hospitalini hapo, Sophia ambaye ni mkazi wa Chanika nje kidogo ya Jiji
la Dar es Salaam ambaye habari zake ziliwahi kuandikwa na gazeti hili
hivi karibuni, amesema anawashukuru wote walioguswa kwa namna moja au
nyingine na matatizo ya watoto wake na kutoa michango ya hali na mali
ili kunusuru maisha yao.
“Nikiri kuwa baada ya gazeti hili kuandika
habari kuhusu mateso ya watoto wangu waliokimbiwa na baba yao, watu
wengi wamejitokeza kuwasaidia, wengine wamenifungulia akaunti yenye jina
la Sophia Rashid Luwingo namba acc/20910000481 NMB.
“Wamesema kwa
kufanya hivyo nitasaidiwa zaidi. Naomba atakayependa kunisaidia atumie
akaunti namba hiyo na sina cha kuwapa, thawabu atawapa Mungu mwenyewe,”
alisema mama huyo na kuongeza kuwa watoto wake baada ya kufanyiwa
upasuaji, wanaendelea vizuri.
Akizungumza na gazeti hili Afisa Ustawi
wa Jamii wa Moi, Mary Ochieng alisema mama huyo amehamishiwa Wodi ya
Makuti Muhimbili kutoka Moi baada ya upasuaji.
“Mimi pia nawashukuru
waliosoma gazeti hili na kumsaidia mama huyu. Sisi kama taasisi ya tiba
tutawasaidia kimatibabu na kuhakikisha afya zao zinaimarika. Nawaomba
watu waendelee kuwachangia kwa kuwa tatizo bado wanalo na hawana uwezo
wowote,”alisema Ochieng.
Alibainisha misaada inayohitajika kuwa ni
pamoja na chakula kwa watoto hao, nguo, fedha na baiskeli ya kumsaidia
mama huyo kubebea watoto wake.
No comments:
Post a Comment