Mdau
wa Sanaa na mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime (kushoto)
akisistiza jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki
nchini kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa
Idaya ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian Shalua na Mkurugenzi wa Idara ya
Utafiti, Mafunzo na Habari Godfrey Mungereza.
Mkurugenzi
wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari BASATA Bw. Lebejo akitoa
ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusu sekta ya muziki nchini.
Rais wa Shindano la Urembo la Miss Utalii Gideon Chipungahelo naye hakuwa nyuma katika kuchangia juu ya tasnia ya muziki nchini. Mzee Kassim Mapili aliwaeleza vijana hali ya tasnia ya muziki ilivyokuwa huko nyuma na mabadiliko yaliyopo sasa
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limevitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa
mbele katika kudhibiti kazi za Sanaa zisizo na maadili kabla ya kwenda
hewani ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Wito huo umetolewa
mapema wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa BASATA Vivian
Shalua wakati akiiahirisha programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kila
wiki kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es
Salaam.
Alisema kuwa, wakati
Baraza limefikia hatua nzuri ya kudhibiti hali hiyo, wadau wakuu katika
kumaliza tatizo hili ni wasanii wanaotakiwa kutunga kazi bora na zenye
maadili huku vyombo vya habari vikiwa na wajibu wa kuchuja kila kazi ya
Sanaa inayopokelewa kabla ya kuirusha hewani.
“Basata
imeshaviandikia vyombo vya habari kuvielekeza kuwa na kamati za ndani za
kudhibiti maadili kwenye kazi za sanaa kabla ya hazijaenda hewani. Hili
ni muhimu sana katika kujenga maadili ya mtanzania” alisisitiza Shalua.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Historia ya Muziki nchini na hatua zake
mkongwe wa muziki wa dansi nchini John Kitime alisema kuwa, kumekuwa na
changamoto mbalimbali miongoni mwa wasanii wa fani hiyo hali
inayoufanya usifike mbali.
Alizitaja baadhi ya
changamoto hizo kuwa ni pamoja na wasanii kutozingatia sheria ya
hakimiliki na hakishiriki iliyopo, kuiga midundo ya muziki kutoka nje
hali inayosababisha kutokuwepo kwa muziki wenye utambulisho wa Tanzania
kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika hususan Afrika Kusini.
“Tatizo kubwa ni
wasanii wetu kuiga miziki na hata tamaduni za kigeni, hatuwezi kuandaa
kazi za Sanaa kufurahisha wazungu au watu kutoka nje tu, tutapotea”
alionya Kitime.
Kwa upande wake Rais
wa Shindano la ulimbwende la Utalii (Miss Utalii) Gideon Chipungahelo
alisema kuwa, kihistoria wanamuziki wetu ukianza na wakongwe waliopo
walijikita katika kuiga miziki ya Zaire hivyo kinachofanywa na wasanii
wetu wa sasa ni mwendelezo tu.
“Ni wazi kazi iliyopo
sasa ni kuwafanya wasanii kujikita katika utajiri mwingi wa makabila
yenye midundo mbalimbali tuliojaaliwa. Hapa ndipo tunapaswa kusisitiza”
alishauri Chipungajelo.
No comments:
Post a Comment