Monday, December 3, 2012

Mpaka wa Tanzania na Malawi wajadiliwa CNN Marekani,yadai ziwa nyasa lote ni mali ya Malawi

*Televisheni ya CNN yaujadili siku nne mfululizo
*Yaonyesha Ziwa Nyasa lote ni mali ya Malawi
*Serikali yaja juu, yawaandikia barua kuwaonya
SERIKALI imekiandikia barua Kituo cha Televisheni cha CNN kinachomilikiwa na Serikali ya Marekani, ikikitaka kituo hicho kukanusha taarifa za upotoshaji zinazofanywa katika mijadala ikionyesha kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi, upo katika fukwe za Ziwa Nyasa, upande wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene, alisema hatua ya upotoshaji inayofanywa na CNN inatakiwa kuachwa mara moja, kwani wanatumia ramani ambayo haitambuliki na vyombo vya kimataifa.
Alisema kwamba, Serikali ya Tanzania haiwezi kuvumilia upotoshaji huo, kwa kuwa unachochea hisia potofu kwa wananchi.
“Hakuna kati yetu asiyejua kuwa Tanzania ipo kwenye mgogoro na Malawi kuhusu mpaka ambao hivi sasa nchi zote mbili zimekubaliana suala hili liende likajadiliwe katika Baraza la Marais wastaafu wa Afrika na chombo hiki kimeundwa na SADC.
“Inasikitisha sana, yaani wakati jambo hili liko katika hatua ya kuelekea katika chombo hicho, CNN wanaendesha mjadala kwa siku nne mfululizo na kuonyesha ramani kupitia televisheni yao, kwamba mpaka wa Malawi upo katika fukwe za Ziwa Nyasa upande wa Tanzania.
“Hili si sawa na hatuwezi kulikubali na katika hali ya kuonyesha kutoridhishwa nalo, Novemba 29 mwaka huu tumekiandikia barua Kituo cha CNN ili kiweze kukanusha upotoshaji wao wanaoufanya.
“Kwa barua tuliyowaandikia, tunaamini watafanya hivyo, kwani haya ni mambo yanayowezekana. Na kama hawatafanya hivyo, tutarudi na kueleza nini tutafanya kwa tukio lao hili la upotoshaji.
“Lakini katika hili, hatua ya kwanza ni kuwaandikia barua na hili tumeshalifanya na pia kitendo cha kuendelea kulijadili jambo hili kwa utashi wako binafsi ni sawa na kutoheshimu vikao vilivyofanyika vya kuwakutanisha viongozi na mawaziri wa nchi zote mbili,” alisema Mwambene.
Novemba 17, mwaka huu, mawaziri na maofisa wa Serikali za Malawi na Tanzania, walikutana nchini na kujadili mgogoro huo. Katika mjadala wao, walikubaliana kuupeleka katika jopo la viongozi wastaafu wanaoshughulikia migogoro ya nchi mbalimbali barani Afrika.
Uamuzi huo ulikuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kuwaeleza waandishi wa habari, kwamba Ziwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu, Tanzania, Malawi na Msumbiji na hivyo si sahihi upande wowote kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya ziwa hilo.
Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, Membe pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Muganda Chiume, walisema viongozi hao wastaafu ndio watakaosaidia kumaliza tatizo hilo.
Waziri Membe alisema kwamba, mapendekezo ya mazungumzo hayo yatapelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Malawi, Joyce Banda, ambao ndiyo watakaopeleka barua katika jopo hilo.
Katika maelezo yake, Membe alisema: “Katika mazungumzo yetu, naweza kusema tumekubaliana na pia hatujakubaliana, hivyo tumeamua kwenda katika hatua nyingine ya usuluhishi ambayo ni kwa jopo la viongozi wastaafu linaloongozwa na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano,” alisema Membe na kuongeza:
“Na endapo jopo hili litashindwa kufikia mwafaka, tutaangalia uwezekano wa kwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ),” alisema.

No comments:

Post a Comment