NASRI SELEMANI
Kupenda
ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu, kwa sababu asilimia kubwa
ya matendo ya mtu huongozwa na mapenzi. Miongoni mwetu kuna watu
wanapenda waume/wake zao, mali, watoto, magari vyakula, vinywaji,
michezo na pengine aina fulani ya maisha.
Baadhi yetu tuko tayari
kupoteza maisha kama tutaachwa na wapenzi au kukosa mambo
tuliyoyapenda. Pamoja na kwamba moyo hupata maumivu pale mazuri
yanapokosekana, bado kuna ukweli juu ya madhara ya kujitakia yanayoweza
kuepukwa na mtu anayeumia kwa kiwango cha kukosa usinginzi, kulia mara
kwa mara kiasi cha kushindwa kufanya kazi zake kama kawaida.
Kupenda
kwa kiwango cha kushindwa kujizuia na kuvumilia ni hatari kwa afya ya
mwanadamu, kwani uchunguzi unaonesha kuwa watu wengi wanaosumbuliwa na
ugonjwa wa vidonda vya tumbo, moyo na wale wenye magonjwa yasiyoonekana
kitalaamu pamoja na wanaokufa ghafla ni athari za msongo wa mawazo
utokanao na kukosa mazuri wanayohitaji katika maisha yao.(Jiulize ni
kipi kinachokutia simanzi moyoni mwako).
Kisaikolojia kuutesa
moyo kwa sababu mpenzi wako kakukataa ni matokeo ya kufikiri vibaya
kwani ushahidi uliopo miongoni mwetu unaonesha kuwa mapenzi si kitu cha
kudumu kwa miaka mingi na anayesema anaweza kupenda jambo moja milele
kwa kiwango kilekile ni mtu anayejiwekea mtengo utakaomnasa mwenyewe na
kumtesa.
Watu wengi tunaowaona wakipagawa baada ya kupewa talaka
na waume zao au kuondolewa mambo fulani waliyokuwa wanayapenda ni wale
walioyachukulia mapenzi kama kitu cha kudumu kisichoweza kubadilika,
huku wakisahau ukweli kuwa wanayopenda kwa wakati huo hawakuzaliwa nayo
na wala hawakuyapenda kabla.
Licha ya kuwepo kwa umuhimu wa
kujiaminisha katika kupenda kwa msingi wa muda mrefu, mtu hatakiwi
kukataa mabadiliko yanapotokea kwani ni wazi kwamba tuliyopenda
tulipokuwa watoto si yale tunayopenda sasa. Hivyo ni jukumu la kila mtu
anayetaka kuwa salama na maumivu ya moyo ya kumkosa ampendaye ni kuwa
tayari kubadilika kutoka kupenda kitu cha awali mpaka kijacho, kuliko
kung’ang’ania wazo moja na kujitesa nalo.
Historia ya mafanikio
ya watu inaonesha kuwa waliokuwa tayari kuacha walivyovipenda na kuanza
mambo mapya ndiyo waliofanikiwa. Mwalimu wangu na bosi wangu Eric
Shigongo aliwahi kuniambia kuwa alilazimika kuondoka nyumbani kwao
Mwanza,akaacha aliowapenda/alivyovipenda kuja Dar es Salaam kutafuta
maisha, leo hii ni miongoni mwa waliopiga hatua.
Katika hali ya
kawaida ni vigumu sana kuondoka miongoni mwa watu uliowazoea, kuacha
makazi yako na kuhamia mkoa mwingine, kuachana na mpenzi wako
mliyeahidiana mambo mengi, lakini mafanikio na usalama wa maisha unataka
mtu awe jasiri wa kupokea changamoto zinazohusu mapenzi.
Ikiwa
umekaa na mwanaume kwa muda mrefu na ukabaini kuwa hana mtazamo wa
kimaendeleo, uwe tayari kukubali mabadiko ya kumwacha na kuanza maisha
mapya.
Msomaji wangu, unaumia kwa sababu mpenzi wako ameamua
kuachana na wewe na sasa unafikiria kujiua, hebu kaa chini ufikirie
kabla ya kuwa na huyo maisha yalikuwa hayaendi? Kama sivyo
kinachokuumiza hasa ni nini mpaka unashinda unalia na kuutesa moyo wako?
Tambua
kuwa dunia ina vitu vingi sana vya kupenda, ambavyo vimeumbwa kwa ajili
ya mwanadamu, usipopenda hiki haina maana hakuna cha kukufaa kipo na
asipokupenda ndugu yako wapo marafiki watakaochukua nafasi ya mapenzi
moyoni mwako na maisha yatasonga mbele kwa mafanikio makubwa,
unachotakiwa ni kujiamini.
Kwa elimu zaidi ya masuala ya maisha na
mapenzi, msaada wa mbinu za kusoma na kufaulu mitihani nunua kitabu
changu cha saikolojia na maisha....
No comments:
Post a Comment