Sunday, October 21, 2012

Mwingine ajifungua akifanya mtihani

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kagemu iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, nusura ajifungue kwenye chumba cha mtihani baada ya kushikwa na uchungu wakati akiendelea na mtihani yake.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwanafunzi huyo, Stella Charles (20), ni kwamba alifanikiwa kukimbizwa hospitalini na kujifungua mtoto wa kike kwa njia ya upasuaji.
Akizungumza na Tanzania Daima katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera, Stella alisema kuwa siku hiyo alikuwa akiumwa jino hali iliyomsababishia maumivu na kwamba hakuwa katika hali yake ya kawaida, “Tangu asubuhi nilikuwa najisikia vibaya, kwanza nilikuwa naumwa jino na nilikuwa nasikia maumivu makali, walimu wakanipa Panadol wakishirikiana na wasimamizi nami nikavumilia niweze kuendelea na mtihani,’’ alisema.
Stella alikiri kuwa alitambua kuwa ni mjamzito na alikuwa akihudhuria kliniki kila mwezi na kwamba walimu wake walikuwa wakijua na kumshauri ajitahidi afanye mtihani.
Alisema kuwa mimba hiyo alipewa na kaka mmoja anayefanya kazi kwenye Kampuni ya mabasi ya Mombasa Raha, lakini mwanaume huyo anaogopa licha ya kuwa anatoa matumizi.
Hata hivyo, alisema kuwa amejifungua kabla ya wakati kwani alitegemea kujifungua wiki mbili baada ya kumaliza mtihani wake.
Alisema awali alikuwa akiishi na kaka yake aliyekuwa akimsomesha tangu darasa la kwanza hadi kidato cha nne, akiwa amemtoa kwao Sengerema na kumleta Bukoba ila kwa sasa anaishi na msamaria mwema. Stella alifafanua kuwa alihama kwa kaka yake baada ya kupata matatizo ya kifamilia ya kutalikiana na mkewe, na hivyo kuoa mke mwingine ambaye ndiye aliyekuwa chanzo cha manyanyaso.
Alisema hali hiyo ilikuwa ngumu kwake akaamua kumuomba rafiki yake, John waliyesoma naye shule ya msingi ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Sekondari ya Bukoba ili amwombee kwa baba yake akaishi kwao wakati akisubiri kufanya mtihani, “Baba yule alikubali kunisaidia baada ya kugundua kuwa ni kabila moja na yeye, yaani Msukuma na hivyo nilihamia huko mwezi wa saba mwaka huu,” alisema.
Afisa Elimu wa Manispaa ya Bukoba, Simon Mwombeki, alikiri kutokea kwa tukio hilo Oktoba 12 asubuhi, akisema mwanafunzi huyo alikuwa akifanya mtihani wake wa mwisho wa vitendo wa baiolojia.

No comments:

Post a Comment