Monday, August 27, 2012

Wanafunzi wambaka mwenzao na kumuua

Polisi mkoani Ruvuma imewatia mbaroni wanafunzi watatu, wawili wa sekondari na mmoja wa darasa la saba wanaosoma katika Shule ya Semeni iliyopo wilayani Tunduru mkoani humo, kwa tuhuma za kubaka na kuua.
Wanafunzi wawili wa sekondari wanadaiwa kumbaka kisha kumnyonga shingo na kumuua mwanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Semeni (jina limehifadhiwa).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimeki, aliwataja watuhumiwa kuwa ni Yusuph Kibwana na Kibwana Adam wote wenye umri wa miaka 18 wanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Kutwa ya Semeni na mwanafunzi wa darasa la saba miaka 15 (jina linahifadhiwa kutokana na umri wake kuwa mdogo), anayesoma katika Shule ya Msingi Semeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Nsimeki, alisema mauaji hayo yalitokea juzi saa 12 asubuhi huko katika kijiji cha Semeni. Alisema inadaiwa siku hiyo Issa Ally ambaye ni mpwa wa mwanafunzi wa kike aliyebakwa aligundua kuwa ndugu yake huyo amebakwa na kunyongwa na watu wasiofahamika na kwenda kutoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi cha Tunduru.
Kamanda Nsimeki alisema baada ya polisi kupokea taarifa hizo walikwenda kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari ambako baada ya kufanya upelelezi wa awali iligundulika msichana huyo alibakwa na kuuawa kwa kunyongwa shingo. Baada ya kufanya uchunguzi wa kina waliwakamata watuhumiwa watatu ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliohusika kumbaka na kumnyonga mwanafunzi huyo. Alieleza zaidi kuwa mtuhumiwa wa kwanza Yusuph Kibwana inasadikiwa kuwa ndiye alikuwa ni mpenzi wa marehemu, wakati Kibwana Adamu inadaiwa kuwa ni rafiki wa karibu wa mtuhumiwa wa kwanza na inaaminika kuwa walishiriki kwa pamoja kumbaka kisha kumuua.
Kwa upande wake mwanafunzi wa darasa la saba inadaiwa kuwa alikuwa rafiki mkubwa wa marehemu na inasadikiwa wakati anabakwa na kuuawa alikuwepo kwenye eneo la tukio lakini alishindwa kutoa taarifa kwenye chombo cha dola.
Kamanda Nsimeki alisema inaendele kufanya upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo na kwamba watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka. Chanzo kingine kilisema kuwa mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.

No comments:

Post a Comment