Polisi mkoani Ruvuma imewatia mbaroni wanafunzi watatu, wawili wa
sekondari na mmoja wa darasa la saba wanaosoma katika Shule ya Semeni
iliyopo wilayani Tunduru mkoani humo, kwa tuhuma za kubaka na kuua.
Wanafunzi wawili wa sekondari wanadaiwa kumbaka kisha kumnyonga
shingo na kumuua mwanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza wa Shule ya
Sekondari ya kutwa ya Semeni (jina limehifadhiwa).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimeki, aliwataja
watuhumiwa kuwa ni Yusuph Kibwana na Kibwana Adam wote wenye umri wa
miaka 18 wanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Kutwa ya
Semeni na mwanafunzi wa darasa la saba miaka 15 (jina linahifadhiwa
kutokana na umri wake kuwa mdogo), anayesoma katika Shule ya Msingi
Semeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Nsimeki, alisema mauaji hayo
yalitokea juzi saa 12 asubuhi huko katika kijiji cha Semeni. Alisema
inadaiwa siku hiyo Issa Ally ambaye ni mpwa wa mwanafunzi wa kike
aliyebakwa aligundua kuwa ndugu yake huyo amebakwa na kunyongwa na watu
wasiofahamika na kwenda kutoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi cha
Tunduru.
Kamanda Nsimeki alisema baada ya polisi kupokea taarifa hizo
walikwenda kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari ambako
baada ya kufanya upelelezi wa awali iligundulika msichana huyo alibakwa
na kuuawa kwa kunyongwa shingo. Baada ya kufanya uchunguzi wa kina
waliwakamata watuhumiwa watatu ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliohusika
kumbaka na kumnyonga mwanafunzi huyo. Alieleza zaidi kuwa mtuhumiwa wa
kwanza Yusuph Kibwana inasadikiwa kuwa ndiye alikuwa ni mpenzi wa
marehemu, wakati Kibwana Adamu inadaiwa kuwa ni rafiki wa karibu wa
mtuhumiwa wa kwanza na inaaminika kuwa walishiriki kwa pamoja kumbaka
kisha kumuua.
Kwa upande wake mwanafunzi wa darasa la saba inadaiwa kuwa alikuwa
rafiki mkubwa wa marehemu na inasadikiwa wakati anabakwa na kuuawa
alikuwepo kwenye eneo la tukio lakini alishindwa kutoa taarifa kwenye
chombo cha dola.
Kamanda Nsimeki alisema inaendele kufanya upelelezi zaidi kuhusiana
na tukio hilo na kwamba watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani
kujibu mashtaka. Chanzo kingine kilisema kuwa mauaji hayo ni wivu wa
mapenzi.
No comments:
Post a Comment