Tuesday, January 22, 2013

Wazazi tujenge tabia ya kuwapa majibu ya kweli watoto

Wazazi wengi wa Kitanzania tuna tabia ya kupuuza maswali tuulizwayo na watoto wetu. Huwa tunahisi ni usumbufu kumjibu mtoto kila swali hasa pale anapokuuliza maswali mengi mfululizo. Hufikia hatua mzazi huanza kumjibu mtoto uongo ili mradi asiumize kichwa kufikiria majibu ya kweli ya kumjibu mwanae.

Tabia hii hufanywa na wazazi wengi bila kujua kuwa mtoto huwa anakiamini sana kile akisemacho mzazi wake.Hivyo hukishika jinsi kilivyo na kuendelea kukua nacho. Itamchukua muda mrefu sana hadi mtoto kuja kutambua kuwa jibu alilompewa na mzazi wake si sahihi.

Mimi nilipokuwa mtoto nilikuwa ninaamini sana kitu ambacho Mama yangu alikuwa akiniambia. Nilikua nabishana kwa nguvu zote pale mtoto mwenzangu aliponipinga juu ya kitu ambacho nilielezwa na Mama yangu.Namshukuru hakuwa akinidanganya.

Wazazi yatupasa kutopuuzia maswali tuulizwayo na watoto wetu.Tuwape majibu ya kweli.Kama hujui jibu sahihi ni bora umwambie utamjibu baadae ili ufanye utafiti kwanza badala ya kumjibu uongo.

Angalizo: Picha niliyo itumia hapo juu ni mfano tu.Msije mkadhani mzazi huyo(Kunambi Jr) ndiye mwenye tabia ya kuwadanganya watoto wake.

No comments:

Post a Comment